RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ametangaza Baraza la Mawaziri lenye wizara 13.
Baraza hilo lina sura mpya nane, likiwajumuisha wajumbe kutoka katika
vyama vya siasa vya upinzani, wanasiasa mashuhuri visiwani humo, huku
naibu mawaziri saba wote wakiwa wageni katika nafasi hiyo.
Akitangaza majina hayo jana, Dk Shein anayeianza awamu ya pili ya
utawala wake Zanzibar, alimtangaza Dk Halid Salum Mohammed, ambaye ni
Mwakilishi wa Jimbo la Donge, kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Katika awamu iliyopita, Dk Halid alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Riziki Pembe Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu, ameteuliwa kuwa Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wakati Moudin Castico, Mjumbe wa Baraza
la Wawakilishi aliyeteuliwa na Rais, anakuwa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji
Wazee, Wanawake na Watoto.
Wengine ni Rashid Ali Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Amani ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo.
Balozi Ali Karume, mmoja wa wanasiasa mashuhuri Zanzibar, ambaye kwa
sasa ni Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais, yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, huku Salama Aboud Talib, ambaye ni
Mwakilishi wa Viti Maalumu na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake
nchini (UWT), akiteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na
Mazingira.
Balozi Amina Salum Ali aliyeshika nafasi ya pili, baada ya Rais John
Magufuli, katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM
mwaka jana, yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko.
Wapinzani ndani
Dk Shein pia amemteua Hamad Rashid Mohammed, ambaye ni Mwenyekiti wa
chama cha ADC, ambaye pia amewahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CUF,
kuwa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.
Hamad pia ndiye aliyeibuka katika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu
wa marudio wa Zanzibar kwa kupata kura 6,734 baada ya Rais Shein
aliyeibuka na ushindi mnono wa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Waziri huyo wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alifuatiwa kwa
karibu na mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata kura
6,076. Viongozi wengine kutoka vyama vya upinzani walioteuliwa katika
Baraza la Mawaziri ni Said Soud Said kutoka AFP na Juma Ali Khatib
kutoka TADEA, ambao wanakuwa mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu.
Mawaziri wa zamani
Mawaziri wanaoendelea na nyadhifa zao ni Haji Omar Kheir aliyeteuliwa
kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za
Serikali, huku Issa Haji Ussi Gavu ambaye katika kipindi kilichopita
alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, amepanda na kuwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Baraza la Mapinduzi.
Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, ameteuliwa
kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Katiba, Sheria na Utawala Bora).
Mohammed Aboud Mohamed ambaye katika kipindi kilichopita alikuwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, anaendelea na wadhifa
wake huo bila ya mabadiliko, huku Mahmoud Thabit Kombo Jecha, ambaye ni
Mwakilishi wa Kiembesamaki akipandishwa kutoka Naibu Waziri wa Afya kuwa
waziri kamili wa wizara hiyo.
Naibu Mawaziri Dk Shein ameteua naibu mawaziri saba wote wakiwa ni
wapya akiwemo Lulu Msham Khamis kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi na Harusi Said Suleiman kuwa Naibu Waziri wa Afya.
Chum Kombo Khamis, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari,
Utangazaji, Utalii na Michezo na Mmanga Mjengo Mjawiri ameteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
Wengine ni Juma Makungu Juma ambaye amechaguliwa kuwa Naibu Waziri wa
Ardhi, Maji, Ujenzi, Nishati na Mazingira, huku Khamis Juma Maalim,
akiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na Mohammed Ahmed Salum
akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.
Waliotemwa
Mawaziri waliotemwa ni pamoja na Dk Mwinyihaji Makame, Mwakilishi wa
Dimani ambaye katika baraza lililopita alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Ikulu na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee.
Mwingine ni Dk Sirra Umbwa Mamboya ambaye katika baraza lililopita
alikuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili na katika Baraza la Wawakilishi
alikuwa Mjumbe wa Kuteuliwa na Rais, ambaye mwaka huu hakupata uteuzi
wowote.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi,
Dk Abdulhamid Yahya Mzee, Rais ataapisha mawaziri wapya na naibu
mawaziri leo Jumapili Ikulu kwa ajili ya kuanza kutekeleza majukumu yao
mapya kwa mujibu wa Katiba.
Lawama za SUK
Baada ya kutangaza mawaziri hao, Dk Shein alisema Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, imekwama kutokana na matakwa ya wananchi na si kikatiba.
Amefafanua kuwa tatizo ni vyama vya siasa ikiwemo CUF, kukacha
kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Marudio Machi 20, mwaka huu
na kusisitiza hatishwi na uamuzi wa chama hicho na vingine vya upinzani
kutoitambua Serikali yake.
“Kukwama kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa si kikatiba ni matakwa ya
wananchi ambao waliamua kupigia Chama Cha Mapinduzi kura nyingi na
kushinda katika majimbo yote ya uchaguzi Unguja na Pemba. “Tatizo hapa
lipo kwa vyama vya siasa vilivyoamua kususia uchaguzi wa marudio ambao
uliitishwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ZEC,” alisema.
Dk Shein alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ameiongoza kwa
miaka mitano, imetekeleza majukumu yake vizuri licha ya kuwepo kwa
hitilafu ndogo ndogo alizoziita ni za kawaida.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo ya kukwama kwa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, iliyotokana na hatua ya makusudi ya CUF ya kutoshiriki
katika uchaguzi wa marudio, Dk Shein amesema hatabadilisha vifungu vya
Katiba kwa ajili ya kuruhusu na kutoa nafasi ya muundo wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa kama ilivyokuwa awali.
Kutambuliwa na Mungu
Alisema hababaishwi na kauli za CUF zilizotolewa na Maalim Seif za
kutoitambua serikali yake na kusisitiza Serikali yake inatambuliwa na
Mungu ambaye ameipa baraka zote pamoja na wananchi wa Unguja na Pemba
ambao ndiyo walioipigia kura kwa wingi na kuipa nafasi ya kushika hatamu
ya madaraka.
“Serikali yangu inatambuliwa na Mwenyezi Mungu kutokana na kudra zake
na anayesema haitambui basi hiari yake, lakini mimi nawapongeza
wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, ambao wamenipigia kura za
ndiyo kwa ajili ya kunipa ridhaa ya kushika hatamu ya kuongoza dola,”
alisema.