MARAIS wanane wa Afrika ni miongoni mwa viongozi mbalimbali kutoka
nje ya nchi, watakaohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya
Tano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Magufuli
ataapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano kesho kwenye Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam. Dk Magufuli (56) alitangazwa mshindi wa Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na
asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, hivyo kumrithi Rais Jakaya
Kikwete katika Ikulu ya Magogoni, ambayo tayari imeshakaliwa na marais
wengine wanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa iliyotolewa jana Dar es Salaam, sherehe za uapisho
zitahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali,
Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda na Wawakilishi mbalimbali
kutoka nje ya nchi. Iliwataja miongoni mwa marais watakaohudhuria
sherehe hizo ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Yoweri Museveni wa
Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Wengine ni Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC), Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na
Rais Edgar Lungu wa Zambia. Taarifa ya Mambo ya Nje ilieleza kuwa Malawi
itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima wakati Namibia
itawakilishwa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje,
Netumbo Nandi-Ndaitwah. Aidha, Serikali ya China itawakilishwa na
Makamu Mwenyekiti wa Chama Tawala.
“Vilevile nchi nyingine ambazo zimethibitisha kushiriki na
zitawakilishwa na kati ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika au Balozi
ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na
Mauritius. “Nyingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa
Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria,
Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan,
Kuwait, Uholanzi na Nigeria,” ilifafanua taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda,
waliothibitisha kushiriki au kutuma wawakilishi wao ni Umoja wa Mataifa
(UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya
ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na
Jumuiya ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).
Wabunge wapya kuwasili Dar Katika hatua nyingine, wabunge wapya
waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam
leo kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk
John Magufuli zitakazofanyika kesho.
Akizungumzia kuwasili kwa wabunge hao, Ofisa Habari Mwandamizi wa
Bunge, Prosper Minja alisema wabunge hao wanatarajiwa kuwasili leo Dar
es Salaam wakiwa na vyeti vyao vya kuteuliwa kuwa wabunge vinavyotolewa
na Msimamizi wa Uchaguzi wa eneo husika.
“Tunategemea kesho (leo), wabunge wapya watawasili kwa ajili ya
kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mteule na tunategemea waje na
cheti hicho pamoja na kitambulisho kingine kinachomtambulisha,” alisema
Minja.
Alisema mara baada ya wabunge hao kuwasili, wanatakiwa kwenda Ukumbi
wa Karimjee kwa ajili ya kutambuliwa na kupewa kitambulisho cha siku ya
sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk Magufuli.
Tamko la Jeshi la Polisi Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini
limejipanga kuhakikisha usalama na ulinzi unaimarishwa wakati wa
kuelekea sherehe za kumwapisha Rais Mteule, Dk John Magufuli.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo,
Makao Mkauu ya Polisi, Paul Chagonja alisema jeshi lake kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya usalama, litahakikisha kunakuwa na usalama wa
raia na mali zao katika kuelekea sherehe za kumuapisha Rais Mteule.
“Niwaombe wananchi kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la
Polisi pindi waonapo vishawishi ama vitendo vyovyote vya uvunjifu wa
sheria,” alisema Kamishna Chagonja. Aidha, Chagonja aliwataka wananchi
kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza
kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
“Jeshi la Polisi linawataka wananchi kote nchini kuendelea kuheshimu
sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya aina yoyote ile ambavyo
vinaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali ikiwemo maandamano
yanayopangwa bila kufuata taratibu,” alisema Chagonja na kuongeza:
“Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu au kikundi
chochote kitakachoonesha viashiria vya uvunjifu wa sheria ama kutaka
kuvuruga amani ya nchi yetu.”
Mbali ya kuwashukuru wananchi na wadau waliotoa ushirikiano
kuhakikisha amani ya Watanzania inadumu katika kipindi cha uchaguzi na
wakati huu wa kuelekea kuapishwa kwa Rais Mteule, alikiri jeshi hilo
kuwashikilia watu kadhaa na baadhi yao kufikishwa mahakamani kutokana na
kufanya makosa wakati wa uchaguzi.
Bila kutaja idadi, Chagonja alisema, “Ni kweli kuna watu kadhaa
tumewakamata kwa makosa mbalimbali wakati wa uchaguzi, kuna wengine
wamefikishwa mahakamani, na kuna wengine bado wanashikiliwa kwa
mahojiano zaidi na wengine wamewekewa dhamana.” Imeandikwa na Ikunda
Eric na Anastazia Anyimike.