Kutangazwa rasmi mshindi wa urais 2015 kutokaa ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar Es Salaam,mh magufuri amepewa cheti.hafla hiyo iliyojumuisha watu mbalimbali wakiwemo jaji mkuu mstaafu mh warioba..na wasimamizi wa uchaguzi wa nje akiwemo mh rais wa nigeria obasanjo.
Friday, October 30, 2015
Thursday, October 29, 2015
Dr. John Pombe Magufuli (CCM) ametangazwa mshindi wa kiti cha Urais Tanzania 2015
Breaking Dr. John Pombe Magufuli (CCM) ametangazwa mshindi wa kiti cha Urais Tanzania 2015, kapata 58%, E. Lowassa 39%
TAARIFA YA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI, OKTOBA 28, 2015
TAARIFA YA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI, OKTOBA 28, 2015
CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wana-CCM na kwa umma: MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA MAJIMBO Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha. MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka. MALALAMIKO YA UKAWA Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote. Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi. Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu. Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi. Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu. January Makamba Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM 28.10.2015
Wednesday, October 28, 2015
Uchaguzi wa Zanzibar wafutwa
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi zanzibar (zec) jecha salim jecha ametangaza kufutwa kwa uchaguzi wa wa serikali ya mapinduzi zanzibar kwahiyo uchaguzi utafanyika baada ya siku 90.
Monday, October 26, 2015
Wednesday, October 14, 2015
Wanafunzi wa vyuo-NEC
TUME ya taifa ya Uchaguzi sasa imethibitisha kuwa wanafunzi wa Vyuo vikuu hawatapiga kura katika uchaguzi mkuu ujao. Akizungumza katika kipindi cha kikaangoni kinachorushwa na EATV, jana Emmanuel Kawishe amesema kuwa wanafunzi hao hawataweza kupiga kura kuchagua diwani,mbunge au Rais kwa kuwa sheria inasema kila mtu atapiga kura pale alipojiandikishia. “Sheria ya uchaguzi kifungu cha 61(3)a kuwa kila aliyejiandikisha atapiga kura alipojiandikisha” alisema Kawishe. Aidha amefafanua kuwa vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1 asubuhi na vitafungwa saa kumi jioni hivyo kuwatahadharisha wapiga kura wote kuwepo kituoni kabla muda wa kufunga. Taarifa ya kutopiga kura kwa wanafunzi wa vyuo vikuu imekuwa rasmi huku viongozi wa Wanafunzi vyuo vikuu wakihangaika kupeleka shauri mahakamani ili serikali ifungue vyuo kwa wakati na kuwapa wao fursa ya kupiga kura. Hii ni mara ya pili kwa Vyuo vikuu kufunguliwa baada ya Oktoba, kwa mara ya kwanza ilifanyika vile vile mwaka 2010 kwa kisingizio cha mikopo ya Elimu ya juu. Ushahidi kutoka kwa wanafunzi mbalimbali waliowahi kunufaika na mikopo wanasema serikali haijawahi kutoa mikopo kwa wakati licha ya sababu za mara kwa mara kuahirisha kufungua vyuo wakati wa Uchaguzi. Mapema mwaka huu, Shirikisho la wanafunzi wa wanachadema wa Vyuo vikuu (Chaso) kupitia Kaimu Mratibu wao Wilfred Mwalusanya aliitaka NEC kueleza utaratibu wa kuwaandisha wanavyuo ili wakati wa kupiga kura waweze kushiriki. Tayari tuhuma zimeanza kutolewa na wadau mbalimbali kuwa tume imetumiwa na serikali ya CCM ili kuinusuru sababu wanavyuo wamehamasika kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
TAMKO RASMI LA BALOZI JUMA V. MWAPACHU.
TAMKO RASMI LA BALOZI JUMA V. MWAPACHU. NAJIVUA UANACHAMA WA CCM
Ndugu zangu, Kesho ni siku muhimu katika kalenda ya Taifa letu. Tunamkumbuka marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetutoka miaka 16 iliyopita. Nadhani ni siku mwafaka kwangu kufanya maamuzi magumu katika maisha yangu ambayo yanahusu uanasiasa wangu. Mimi ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 1967 wakati nilipojiunga na TANU Youth League. Nimepata fursa ya kuwa kiongozi ndani ya Chama hiki. Lakini kuanzia kesho mimi si mwanachama wa CCM tena. Natoa maelezo yafuatayo: Kwa kipindi chapata mwezi na nusu hivi sasa mmekuwa mkisoma makala zangu kuhusu msimamo na mwelekeo wangu katika masuala ya siasa za hapa nchini hususan kuhusu uchaguzi mkuu na mstakabali wa demokrasia nchini mwetu. Nyote mnatambua kwamba kuanzia mchakato wa kumpata mgombe wa Urais ndani ya CCM kule Dodoma, ambako nilipiga kambi, sijayumba katika msimamo wangu kwamba Edward Ngoyai Lowassa ndiye chaguo langu katika kampeni za kumpata Rais mpya wa Taifa letu. Chaguo langu si ndoto wala mlipuko wa mapenzi juu ya Lowassa. Nimemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 nikiwa cadre wa Chama cha Mapinduzi kwa mahusisho katika majukumu ya Kic,ssa amejaaliwa nuru na uwezo wa kuongoza na wa kupendwa na watu. Ni msikivu pamoja na kwamba ni kiongozi asiyependa ukiritimba na utovu wa nidhamu, iwe kwa upande wa watumishi au wananchi wenyewe. Kubwa kwake ni ucha Mungu wake ambao unamsaidia sana katika uongozi unaojali na kuheshimu utu, ukweli na uwazi. Wanaodhani au kutaharuki kwamba eti anaweza au ana hulka ya kulipiza kisasi kwa jambo lolote lile ni waongo; wanajilinda. Lowassa ni chaguo la wengi na CCM, katika busara yake ya kumuengua katika mchakato wa kumpata mgombea wa Urais, kimedhihirisha kutokuwa Chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia. Dalili za Chama hiki kupoteza lengo la kuwa Chama cha watu, na kuwa cha viongozi wachache zilianza siku nyingi na hasa katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. CCM kimebadilika na kuwa Chama cha makundi na migawanyiko yakupambana, si kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa Chama, bali ya kumalizana na kutaka kufukuzana. Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi tu iliyopita! Aliweza kushinda vita hivyo kutokana na kupendwa na wengi ndani ya CCM. Hivyo, kujitoa kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM si Chama tena cha watu. Kimetekwa. Na mimi nakubaliana na msimamo wa Lowassa na hao waliyofuata kutoka nadani ya CCM. Niliwahi kuandika makala katika ukurasa huu nikimnukuu mshairi mmoja wa Uingereza aliyeandika kwamba, ‘there comes a time when the door opens and allows the future in’. Mlango huo sasa umefunguka usoni mwangu na huu uamuzi wangu maana yake ni kukubali kwamba wakati mpya umewadia; ni wakati wa mabadiliko. Kuendelea kujihisi kwamba ningali mwana CCM wa kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe. Si sawa. Kama marehemu Baba wa Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama yangu’. Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni, Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na Chama kingine. Mwenyezi Mungu anilinde.
Thursday, October 08, 2015
Bado masaa kadhaa Fainali ya BSS..
FAINALI YA BSS ITAFANYIKA KESHO KWA MUJIBU WA VIONGOZI WA BSS
![]() |
| Angel kato mshiriki katika fainali ya bss |
![]() |
| Frida amani mshiriki wa Fainali ya BSS |
![]() |
| Nasibu fonabo mshiriki wa Fainali ya bss |
maelfu wajitokeza kumuaga Mchungaji Mtikila
RAIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji pamoja na viongozi wa kitaifa, katika kumuaga Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila aliyekufa kwa ajali hivi karibuni mkoani Pwani.
Katika shughuli hiyo, viongozi wengi waliohudhuria walimuelezea Mtikila kuwa ni mwanaharakati wa mageuzi, aliyeipigania Tanganyika mpaka kifo chake, lakini pia alisimamia na kuheshimu taratibu za kisheria na kutaka mabadiliko bila uoga.
Rais Kikwete alifika katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, akiambatana na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Msajili wa zamani wa vyama hivyo, John Tendwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
Pia walikuwepo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha PPT-Maendeleo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Dotnata Rwechungura.
Akizungumza katika shughuli hiyo ya kumuaga Mtikila ambaye jeneza lake lilifunikwa kwa bendera ya Tanganyika, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mutungi aliwataka watanzania kumuenzi mchungaji huyo kwa matendo yake ya kuchukia vurugu na badala yake aliamini zaidi katika sheria.
“Mchungaji Mtikila atakumbukwa kwa misimamo yake mikali. Alipenda kusimamia kile anachokiamini. Lakini kubwa zaidi alitoa mchango katika nyanja ya Sheria, kwa sasa huwezi kuzungumzia masuala ya sheria hususani haki za binadamu bila kumtaja Mtikila,” alisema Mutungi.
Alisema kupitia sekta ya Sheria, mwanaharakati huyo alifanikisha mabadiliko kadhaa, ikiwemo kuingizwa kwenye Katiba kwa kifungu kinachoruhusu mgombea binafsi, lakini pia alifanikisha kubadilishwa kwa kifungu kinachohusu maandamano.
“Huyu alikuwa ni mpambanaji, alifungua kesi nyingi kwa kuwa aliamini katika kufuata sheria na si kuandamana au kufanya vurugu. Naomba tumuenzi kwa kutopenda kushinikiza fujo na maandamano, vyombo vya sheria vipo kama kuna tatizo tuvitumie kutafuta haki,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Dk Bilal alimtaja Mchungaji Mtikila kuwa alikuwa ni mtu jasiri, aliyeshirikiana na wenzake bila kujali tofauti za mitazamo waliyonayo. “Mimi nilimfahamu Mtikila kupitia uanaharakati wake wa kutaka mabadiliko, ni kweli alikuwa anataka sana kuirejesha Tanganyika, lakini pamoja na tofauti za fikra zetu, alikuwa anakuja hadi ofisini kwangu kipindi kile nilikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia na tulikuwa tunazungumza sana,” alisema.
Aliwataka watanzania kuiga mfano wa matendo ya Mtikila, kwani kwa sasa nchi inataka watu kama hao wenye mawazo mapya na hawaogopi kuyatoa na kuyatetea bila kudharau mawazo na fikra za wengine.
Maalim Seif, kwa upande wake, alisema alifahamiana na Mtikila kupitia harakati zake za kisiasa na kubainisha kuwa ni mtu anayejiamini, asiye uoga na mwenye kuajimini na kusimamia kile anachokiamini.
Mziray alisema anaipongeza Serikali kwa kitendo chake cha kushirikiana na familia ya Mtikila kwa hali na mali, bila kujadili kuwa ni mwanaharakati wa mabadiliko, jambo alilosisitiza kuwa hiyo ndio Tanzania inayotakiwa kwa sasa.
Makamu Mwenyekiti wa DP, Peter Mwagila alibainisha kuwa chama hicho kimepata pigo na pengo kubwa kwa kuondokewa na mwenyekiti wao, ambaye pia pamoja na kuwa muasisi wa chama hicho, ni mwanaharakati wa mageuzi aliyepigania nchi yake ya Tanganyika.
“Mtikila ndoto zake zilikuwa ni kurejeshwa kwa Tanganyika ambayo iliondolewa kwenye ramani ya dunia tangu mwaka 1962, alitaka kuwepo na Rais wa Tanganyika, Katiba, wabunge na mamlaka zote za nchi ya Tanganyika. Lakini pia alipinga rushwa, ufisaidi na kuwachukia viongozi wanaojilimbikizia mali,” alisema.
Alisema chama hicho kitahakikisha kinaendeleza na kusimamia harakati zote zilizoanzishwa na Mtikila ikiwemo kuidai Tanganyika. Msemaji wa familia ya mchungaji huyo, Peter Mayani, wakati akisoma wasifu wa Mtikila, alisema mwanaharakati huyo alibobea katika fani za sheria, uchumi na masoko na aliwahi kuajiriwa Mahakama Kuu na Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, ambalo alilitumia kutoroshea wanaharakati wa chama cha Frelimo.
Alisema Mtikila aliokoka rasmi mwaka 1983 na kuanzisha Kanisa la Pentekoste la Full Salvation na mwaka 1990 alianza harakati za ukombozi, zilizoshinikiza kuanzishwa kwa vyama vingi mwaka 1992. Pia alianzisha chama cha DP, ambacho kilichelewa kupata usajili wake hadi mwaka 2000.
Mtikila baada ya kuagwa alisafirishwa kwenda kijijini kwao Milo, wilayani Ludewa mkoani Njombe ambako anatarajiwa kuzikwa leo. Marehemu ameacha mjane Georgia Mtikila. Askofu wa Kanisa la Ufunuo, Nabii Paul Bendera, aliwataka watanzania kutambua kuwa wote ni wageni duniani na kwamba kila mtu bila kujali ni nani duniani na ana cheo gani iko siku yake atakufa.
“Kwa sasa hali imekuwa ngumu na mbaya nawaomba ndugu zangu tuwe makini, lakini kubwa zaidi kila mtu amheshimu maisha ya mwenzake tuweke upendo na amani mbele na hii iwe ndio kipaumbele chetu. Naomba Serikali nayo iongeze juhudi za kuwalinda wananchi wake,” alisisitiza.
Mchungaji Daudi Mwaijojele, alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kuacha uchafu na kumrejea Mungu, ili kutengeneza maisha yao ya baadaye pindi watakapokufa. “Nawaomba acheni uchangudua, ufisadi na michepuko tena hiyo michepuko ndio inaleta magonjwa kama vile Ukimwi majumbwani na kusambaratisha familia,” alisema.
Mtikila alikufa kwa ajali ya gari aina ya Toyota Corolla, lenye namba za usajili T 189 AGM maeneo ya Msolwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani. Alikuwa akitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.
Subscribe to:
Comments (Atom)






