Monday, September 28, 2015

Marekan yaridhia Mabilioni

MCC Yaiondolea vikwazo Tanzania


Rais Jakaya M.Kikwete
TANZANIA imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani, hivyo itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Habari hizo njema zilitangazwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC.

Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. “Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania, imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2 ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Hyde alimwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
Hyde alimwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na tatizo hilo.
MCC ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na rushwa.
Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.
Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC, Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI), Balozi Mark Green.
Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1. Hyde alisema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi.
Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1. Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa Dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na Sh bilioni 992.80).
Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1, Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya mpango huo, na kwa kupita MCC-2, Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani. Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea- Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.

Friday, September 18, 2015

Mabasi Yaendayo Haraka kuanza kazi oktoba 2


 HATIMAYE mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Oktoba 2 mwaka huu kwa njia moja.
Aidha, wamiliki wa magari, pikipiki na baiskeli ambao watakutwa wakitumia barabara ya mabasi ya haraka, kama maegesho watapewa adhabu kali ya faini au kifungo gerezani.
Hayo yalibainishwa jana na Ofisa wa Fidia wa Wakala wa Usafiri Haraka wa Mabasi (DART), Deo Mutasingwa baada ya wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya ziara ya kujionea jinsi huduma hiyo itakavyotolewa.
Alisema huduma hiyo ambayo ni ya muda na kufanywa kwa kipindi cha miaka mwili, itakayofanywa na Kampuni ya UDA, itaanza Oktoba 2 mwaka huu kwanjia moja ya kutoka Kimara hadi Kivukoni yenye urefu wa kilomita 20.9.
Alisema kwa njia za barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi eneo la makutano ya Morocco jijini Dar es Salaam, itaanza kutumika baada ya miundombinu yake kukamilika.
Alisema katika mradi huo wa muda wa miaka miwili, mabasi 100 yatakayoendeshwa na madereva 200 yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo.
Aidha, Mutasingwa alisema wenye magari, pikipiki baiskeli ambao watakutwa wakitumia barabara hizo au kuegesha vyombo vyao watatozwa faini ya kati ya sh 250,000 hadi sh 300,000 au kifungo cha miaka miwili jela au adhabu zote kwa pamoja.
“ Tumekuwa na changamoto kwa watumiaji wengine wa barabara, jambo ambalo linaleta uharibifu na pia kuingilia safari. Tumeshazungumza na wenzetu wa halmashauri kushughulikia hili, hivyo kuanzia mwezi ujao atakayekutwa akitumia barabara hizo au kupaki chombo chake adhabu kali itakuwa juu yake,” alisema.
Alipoulizwa suala la nauli, alisema hilo liko kwenye mchakato kati ya DART, wamiliki wa mabasi na walaji lengo ni kuja na nauli ambayo haitamuumiza mwananchi lakini pia yule anayeendesha apate faida.
Alisema wakati utoaji wa huduma hiyo utakapokuwa kamili, watanzania takribani 300,000 watahudumiwa kwa siku.
Msimamizi wa Mifumo wa DART, Junn Mlingi alisema vituo vikuu vya mabasi vitakuwa na miundombinu ya kumwezesha mtumiaji yeyote kama ni mgeni, mlemavu wa viungo kuona au kusikia kuweza kupata huduma hiyokwani kutakuwa na matangazo ya sauti na maandishi.
Alisema mabasi hayo yatakuwa yakiendeshwa kwa kilomita 50 kwa saa kwa mwendo wa kasi na kilomita 24 kwa saa kwa mwendo wa wastani.“

Tuesday, September 08, 2015

Dk John Magufuli jinsi alivyoshambulia jukwaa Morogoro

 MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema Serikali atakayoiongoza itajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kuongeza ajira na mapato ya Serikali, huku akiwaahidi wakazi wa Morogoro kufufua viwanda vyao.
Amesema hayo katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika moja ya mikutano mikubwa ya kampeni za uchaguzi, uliorushwa moja kwa moja na televisheni mbalimbali nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Magufuli alisema mbali na kujenga viwanda, pia Serikali hiyo itatoa Sh milioni 50 kwa kila mtaa na kijiji kwa ajili ya wanawake na vijana kukuza mitaji yao ya biashara na kuanzisha biashara mpya, huku akiwahakikishia kutobughudhiwa.
Kuhusu elimu na afya, Dk Magufuli alisema kuanzia mwakani wanafunzi kutoka darasa la awali mpaka kidato cha nne, hawatalipa ada ya shule kwa kuwa Serikali atakayoiongoza itatoa huduma hiyo bure. Pia, alisema atashusha bei ya vifaa vya ujenzi ili wananchi wanaofanya kazi na biashara na kujipatia kipato halali, wajenge nyumba kwa gharama nafuu.
Kabla ya Dk Magufuli kuhutubia, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipanda jukwaani na kusema akistaafu kwa kumkabidhi nchi Dk Magufuli, atalala usingizi.
Rais Kikwete alisema hakwenda mkoani huko kuhudhuria mikutano ya Dk Magufuli, bali alikwenda kuhudhuria kikao cha mkakati cha Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kilichofanyika mkoani humo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kwa kuwa mgombea huyo alikuwa na ratiba ya kuhutubia mkutano katika uwanja huo, akaona ni vyema na yeye ahudhurie mkutano huo.
Alipopewa nafasi ya kumkaribisha mgombea huyo, Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuzungumza kidogo kilichofanyika Dodoma, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho.
Alisema walitumia muda mrefu kujadili kila mgombea kati ya wagombea 38 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, mpaka wakapata wagombea watano akiwemo Dk Magufuli, Balozi Amina Salum Ali, Dk Asha-Rose Migiro, Bernard Membe na January Makamba.
Baada ya hapo, alisema walikwenda katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ambako wafuasi wa mmoja wa wagombea ambaye hakuingia katika tano bora, Edward Lowassa, walipewa nafasi kubwa ya kuzungumza baada ya mgombea huyo kutopenya tano bora.
Kwa mujibu wa Kikwete, walizungumza yote na sababu ya kupata wagombea hao na sifa zao dhidi ya za wenzao na wakaafikiana na kupiga kura, ambapo Lowassa ambaye baadaye alitoka na kuhamia Chadema, alipiga kura.
Baada ya hapo walipatikana watatu, Magufuli, Balozi Amina na Dk Migiro ambapo katika Mkutano Mkuu, alipita Magufuli ambaye alisema ana kila sifa ya kuwa rais na kuongeza kuwa wananchi walisema yeye Kikwete ni mpole, hivyo baada ya kupata rais mpole, Tanzania inahitaji rais mkali.
Rais Kikwete alisema kampeni zinavyokwenda, anaona baada ya Uchaguzi Mkuu vyama vya upinzani vilivyojiunga katika mwavuli wa Ukawa, vitageuka jina na kuwa Ukiwa

Flaviana Matata ateuliwa kuwa Balozi wa hiyari wa Utalii nchini Marekani




Mwanamitindo wa Kimataifa anaefanyia kazi zake za nchini Marekani Flaviana Matata amechagulia na


Wizara ya Maliasili   kuwa Balozi wa Hiyari ‘Good Will Ambassador’ kwa kipindi cha miaka mitatu kwa dhumuni la kutangaza  vivutio vya utalii vya Tanzania ndani na nje ya nchi.
Flaviana ambaye juzi alikuwa mmoja kati ya shuhuda wa kushuhudia wizara ya maliasili na utalii wakizindua rasmi tangazo litakalokuwa linatangaza vivutio vya Tanzania nje ya anchi alitawazwa leo hii na katibu mkuu Dr Adelhelm James Meru aliyemkabidhi kwa niaba ya Waziri , Mheshimiwa Lazaro Nyalandu huku Kaimu Mkurugenzi Madam Devota Mdachi akishuhudia