CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua kampeni zake jijini Dar es Salaam
 |
| Mwana muziki Bwana misosi, akitoa burudani katika uzinduzi wa kampeni wa
Chama cha ACT-Wazalendo uliofanyika viwanja vya Zakhem Mbagala Dar es
Salaam jana. |
 |
| Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira akihutubia katika uzinduzi wa kampeni ya chama hizo
uliofanyika viwanja vya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam jana. |
 |
| Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, akigawa ilani ya chama hicho kwa mgombea urais na mwenza wake |
 |
| Mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo akihutubia kwenye uzinduzi huo. |
CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua kampeni zake jijini Dar es Salaam
kwa kuahidi kitakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitaunda serikali ya
Umoja wa Kitaifa. Aidha katika uzinduzi huo ambao viongozi mbalimbali wa
chama hicho walihutubia, Mgombea Urais wa chama hicho Anna Mghwira
alisema wananchi wakimpa ridhaa, waziri mkuu wake atakuwa Zitto Kabwe.
“Nitakapounda serikali, katika katiba, mtu wa kwanza kusaidiana na
rais licha ya makamu, ni Zitto Kabwe, atakuwa Waziri Mkuu katika
serikali ya kwanza,” alisema Anna Mghwira ambaye pia alisema atahusisha
viongozi waadilifu kutoka CCM, Chadema na vyama vyote vya siasa na
taasisi zote kiraia.
Akihutubia mkutano huo uliofanyika viwanja vya Mbagala Zakhem,
mgombea huyo, katika kuelekeza nia yake ya kuunda serikali hiyo ya
umoja, alisema linapokuja suala la kitaifa, hakuna haja ya kuangalia
masuala ya itikadi. “Mimi ni mama, hukusanya watoto wake.
Hata mama wa vifaranga hukusanya vifaranga pamoja na kuviweka kwenye
mbawa zake…mimi nina mbawa za moyo…nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa
itakayotokana na sekta binafsi lakini kutoka watu wazalendo, wenye utu,
waadilifu, taasisi za kijamii, mashirika ya kidini, makundi ya umma ili
kuunda taswira ya nchi yetu.”
Mghwira alisema taifa linahitaji mabadiliko si ya tu kifikra na
kisera, bali pia ya kijinsia kwa kumchagua yeye kuwa Rais wa nchi.
Alisema chama chake kinatilia mkazo utu, uzalendo na uadilifu.
Makao makuu Dodoma Aidha alisema, Serikali itakapoundwa itaapishwa
Dodoma na watahakikisha wanarudisha kazi kubwa aliyoifanya Rais wa
Kwanza, Julius Nyerere ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na
serikali lakini siyo makao makuu ya chama.
Alisema kuweka mji huo makao makuu, maana yake ni kuleta watu wote
kutoka pande zote za nchi. Vipaumbele Alitaja vipaumbele vyake ni kuwa
na mfumo imara na endelevu wa hifadhi ya jamii unaojengea uwezo wananchi
kukabiliana na majanga. Alisema asilimia sita pekee ya Watanzania
wanafaidika.
“Tutatumia hifadhi ya jamii kama nyenzo ya kukuza akiba nchini ili
kuwe na vyanzo vya mitaji ya uwekezaji wa ndani…tutapanua hifadhi ya
jamii kufikia makundi yote katika jamii ikiwamo wakulima, wafugaji, mama
lishe na bodaboda,” alisema. Kipaumbele kingine alichoahidi ni uchumi
shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora.
Alisema watu wengi hawana uhakika na maisha yao kimapato. Aidha
alisema, watajikita kwenye uwekezaji wa kilimo na kusimamia uzalishaji
wake. Aidha, aliahidi kuhakikisha ardhi na mashamba yote yaliyo chini ya
mashirika ya umma, yanachukuliwa na kuwekwa chini ya uzalishaji mdogo.
Kwa upande wa viwanda, alisema atahakikisha bidhaa zinazozalishwa
nchini zinaongeza mapato ya fedha za kigeni. Chama hicho kupitia kwa
mgombea, kimesema kitaweka msukumo kwenye bidhaa za nguo na vitakuwapo
viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.
Vipaumbele vingine ni kuhakikisha madini, mafuta na gesi, vinakuwa
mali ya wananchi kikatiba. Kuhusu Katiba Mpya, alisema wataruhusu Tume
ya Jaji Warioba imalize kazi ya katiba ilikoishia. Mgombea huyo
aliendelea kutaja vipambele vyake kuhakikisha anaboresha huduma za afya
ikiwamo kudhibiti vifo vya mama na mtoto.
Aliahidi kuondoa tatizo la watoto wa mitaani. Misamaha ya kodi kwa
mujibu wake, haitazidi asilimia moja ya pato la taifa na wakati huo huo
atadhibiti mianya ya ukwepaji kodi hususani kwa kampuni za kigeni.
Sifa za rais Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo,
alishauri wananchi kuangalia wagombea urais kama wanalinda haki za
walio wengi au ni mateka wa matajiri. Mkumbo alisema, kiongozi mkuu wa
nchi, kwa maana ya rais, ana kazi kuu nne ambazo ni fikra na kutoa dira
ya nchi jambo ambalo anapaswa kuwa na uwezo wa kufikiri.
“Tatizo ni kufikiri na kutoa dira ya nchi…tunataka rais atakayetoa
misingi ya nchi, atatuletea sera..,” alisema Kitila. Alisema kazi ya
pili ya rais, ni kuwa mlinzi mkuu wa tunu za taifa huku akisisitiza
katika tunu ya umoja, wananchi kuepuka mgombea mwenye tabia za kidini,
kikabila na kikanda.
“Rais ndiye mlinzi wa usawa katika taifa…,” alisema na kushauri
wananchi kuangalia wanaogombea kama wanaelekea kulinda haki za walio
wengi au ni mateka wa matajiri. Alitaja tunu nyingine ni muungano kwa
kusema anayeomba urais na kutaka kucheza na muungano lazima akataliwe.
Kuhusu uadilifu, alisema inapaswa aingie rais atakayekoleza vita ya
ufisadi . “Kama kuna mtu anataka urais hata kutamka neno ufisadi
anaogopa, huyu hatufai hata kidogo,” alisema Kitila.
Akizungumzia demokrasia, alisema nchi imepiga hatua katika demokrasia
ambayo inahitaji rais atakayeipeleka mbele. Vile vile alisema katika
kuchagua, ni lazima kuangalia mgombea ndani ya chama chake
alipatikanaje.
“Kazi nyingine ya rais lazima awe mfano wa binadamu bora katika
jamii. Hatumaanishi malaika, tunamaanisha kwamba popote atakapoenda,
akisimama wajue huyu ni Mtanzania, awe sura ya utaifa,” alisema na
kusisitiza sifa nyingine ya rais itokane na uadilifu wa chama chake.
Kitila alisisitiza, “Mtu asiye mlaghai lazima aliyotuambia jana, na
leo yafanane. Akihubiri maji lakini yeye anakunywa wiski, yeye ni
mlaghai. Akituambia ni nyeusi jana, leo nyekundu, kesho nyeupe, huyo ni
mlaghai.” Alisisitiza kuwa ACT Wazalendo inazingatia misingi na sera
huku akibeza vyama vingine kwamba vinauza mbwembwe na ulaghai.
Ukawa wasutwa Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni, Habib Mchange,
aliisuta Chadema na CUF kupitia viongozi wao akirejea mkutano wa Mwembe
Yanga mwaka 2007, walipotaja orodha ya waliowatuhumu kuwa mafisadi papa.
“Kipindi kile hawakuwa na Ukawa bali walikuwa na ushirikiano.
Walitaja watu wanaofilisi taifa hili ambao ni watu kumi na moja…kati
ya watu hao waliotajwa kuwa ni mafisadi, namba tisa alikuwa ni Lowassa,”
alisema Mchange. “Tulikubaliana 2007 kwamba tunapambana na CCM na wana
mafisadi. Leo naomba mtafakari…ili tusiwe wajanja wajanja lazima tuseme
ukweli.
Unayosema jana ndo hayohayo uyaseme leo,” alisema. Akinyoshea CCM pia
vidole, Mchange alilinganisha mgombea wa Ukawa sawa na chupa yenye sumu
iliyobandikwa jina la maji. Alinadi chama chake akisisitiza wananchi
wakiamini kwa kuwa kimekuja katikati ya sumu mbili za CCM na Ukawa.
Amshangaa Sumaye, Lowassa Mchange alisema anachoona ni kwamba,
ufisadi uliokuwa CCM, umezaliana na kutanuka na hatimaye kuhamia Ukawa.
“Jana (juzi) Sumaye ametulaghai… Anasema anashangaa kwa nini CCM
inaendelea kuaminiwa,” alisema.
Alikumbusha kuhusu mjadala wa kununua ndege ya rais ambayo ilipigiwa
kelele, kwamba wakati huo Sumaye ndiye alikuwa Waziri Mkuu. Pia kuhusu
ahadi ya Lowassa ya kumwachia huru mwanamuziki Nguza Viking maarufu kama
Babu Seya, Mchange alieleza kushangazwa naye kutokana na kile
alichosema, wakati anafungwa, ndiye alikuwa Waziri Mkuu.
Mchange alikuwa mkali zaidi katika hotuba yake hasa alipokuwa
anazungumzia ufisadi na wizi. “ Kumbe unaruhusiwa kuwaibia Watanzania
ukiwa CCM ukirudi upinzani ni msafi. Mwizi ni mwizi tu.
Fisadi ni fisadi tu…Wanatudanganya kwamba kuna Ukawa…waongo. Ukawa
wanatafuta rais tu. Ukawa huku chini kwa wapiga kura haupo,” alisema
Mchange. Alihoji ni namna gani mgombea urais ataweza kunadi wagombea wa
vyama vinavyounda Ukawa ambao wamegoma kuachiana majimbo hususani Jimbo
la Tabora Mjini, Serengeti na Segerea.
“Sasa tuwaulize Ukawa Lowassa akipita Tabora mjini atamnadi nani?,”
alisema akimaanisha mgombea wa CUF na Chadema wanaogombea jimbo hilo.
Zitto Kabwe Alisema ACT Wazalendo wanarejesha miiko ya uongozi.
Alisisitiza kuhusu utaratibu wa chama chake wa kiongozi kutangaza
mali na madeni yake. Zitto alisema kila chama kinachogombea, kinasema
kitapambana na rushwa na ufisadi bila kueleza ni namna gani watapambana
tofauti na ACT Wazalendo ambacho kimesema kitapambana kwa kurejesha
miiko ya uongozi.
Alihoji ni namna gani mawaziri wakuu wastaafu wanatamba kuleta
mabadiliko. Zitto alimsuta Sumaye akisema, wakati ATCL inauzwa aliyekuwa
Waziri Mkuu ni Sumaye na wakati huo huo na mwaka 2007 ilipotaka
kufufuliwa wakapewa Wachina ambao walisababisha hasara kwa taifa
aliyekuwa Waziri Mkuu alikuwa Lowassa.
Zitto alikosoa pia kauli ya Magufuli juu ya ahadi yake ya kuanzisha
mahakama ya kupambana na rushwa, akisema kwenye katiba mpya, kulikuwa na
kipengele cha kuipa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
mamlaka ya kukamata na kushitaki wala rushwa lakini CCM waliikataa.
Kuhusu ufisadi, Zitto alisema hakuna chama cha siasa chenye uwezo wa
kupambana nao isipokuwa ACT Wazalendo. Akitumia kete ya jinsi kumnadi
mgombea, Zitto alisema, ni wakati wa Watanzania kumpa mwanamke uongozi
wa nchi ikizingatiwa miaka yote, imekuwa ikiongozwa na wanaume.